Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesisitiza ufanyike uchunguzi
huru na wa kimataifa juu ya kudunguliwa ndege ya shirika la ndege la
Malaysia katika anga ya Ukraine na kuwaua abiria wote 298

Wanachama wa Baraza hilo wametaka wachunguzi wa kimataifa kupewa nafasi ya kuingia eneo la ajali na kufanya uchunguzi huru unaoendana na viwango vya kimataifa.
"Tunaomboleza vifo vya raia wetu 9 waliokuwamo ndani ya ndege hii. Huu
ni wakati mgumu kwa jamii ya kimataifa. Hili litahitaji uchunguzi wa
kimataifa unaoendana na muongozo wa mamlaka wa usafiri wa anga," alisema
Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Mark Lyall Grant
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk
ameielezea ajali hiyo kuwa "uhalifu wa kimataifa" ambao walioufanya
wanapaswa kuadhibiwa katika mahakama ya kimataifa."Huu ni uhalifu dhidi ya binaadamu, kila mtu anapaswa kuwajibishwa, namaanisha kila mtu anayewaunga mkono hawa magaidi ukiwemo utawala wa Urusi," alisema Yatsenyuk.
Familia za walioangamia waelezea masikitiko yao

Familia za walioangamia wamekusanyika katika uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur, na Schiphol Uholanzi wote wakisubiri habari zaidi juu ya kile kilichotokea katika mkasa huo.
Akmar Mohamad Noor, aliye na umri wa miaka 67 kutoka Kuala Lumpur anasema dadake alikuwa anarejea nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano kuitembelea familia. Amesema kabla ya kuabiri ndege dadake alimpigia simu na kumuambia wataonana muda mfupi ujao, lakini hilo halikuezekana.
Huku hayo yakiarifiwa Rais wa Urusi Vladimir amesema anawasiliana na mwenzake wa Ukraine Petro Poroshenko na kutoa matumaini kuwa mgogoro wa Ukraine unaoaminika kuchangia pakubwa katika kudeguliwa kwa ndege ya shirika la Malaysia utapatiwa suluhisho.
Lakini kwa upande wake kiongozi wa waasi wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine ameondoa uwezekano wa kufikia msimamo wa pamoja na Ukraine wa kusimamisha mapigano kwa muda lakini akasema watatoa nafasi kwa wachunguzi kuingia eneo ilipoanguka ndege hiyo ya Malaysia.
No comments:
Post a Comment