![]() |
| Viongozi wa nchi za BRICS wakiwa Fortaleza, Brazil . (15.07.2014) |
Viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi BRICS yameanzisha benki ya
maendeleo yenye thamani ya dola bilioni 100 katika hatua ya kuubadili
mfumo wa fedha wa kimataifa unaohodhiwa na mataifa ya magharibi.
Viongozi wa mataifa ya BRICS pia wameunda mfuko wa akiba utakaokuwa na uwezo wa dola bilioni 100 kukabiliana na shinikizo za kifedha.Benki hiyo ilokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu itaitwa Benki ya Mpya ya Maendeleo.
Hayo ni mafanikio ya kwanza makubwa ya nchi zinazounda BRICS za Brazil,Urusi,India,China na Afrika Kusini tokea zilipokutana mwaka 2009 kushinikiza kuwa na sauti kubwa katika mfumo wa fedha duniani ulioanzishwa na mataifa ya magharibi baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kujikita katika Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na Benki ya Dunia.
Ushawishi wa BRICS
Mataifa hayo yanayoinukia kiuchumi yalilazimika kuratibu hatua hiyo ya pamoja kufuatia kuhamishwa kwa mtaji kutoka katika nchi zinazoinukia kiuchumi mwaka jana kulikosababishwa na hatua za kuchochea uchumi za Marekani.
Benki hiyo mpya inaonyesha kuongezeka kwa ushawishi wa mataifa hayo yanayounda BRICS ambayo kwa jumla yana nusu ya idadi ya watu duniani na pato la kiuchumi duniani la takriban asilimia 20.
Mbadala wa ushawishi wa Marekani
Rais Dilma Rousseff wa Brazil ameweka wazi uwezekano wa kutumia fedha za benki hiyo kuzisaidia nchi nyengine ambazo sio wanachama wa BRICS.
Leo viongozi wa mataifa hayo ya BRICS watakuwa na mkutano wa kilele na marais wenzao wa Amerika Kusini kutafuta njia mbadala za kukabiliana na ushawishi wa Marekani katika eneo hilo la Amerika Kusini.
Mataifa yatakayohudhuria mkutano huo ni pamoja na Argentina,Chile,Colombia, Ecuador na Venezueala.

No comments:
Post a Comment