NI ukweli ulio wazi kwamba kumekuwako na
ongezeko la idadi kubwa ya vijana wanao hitimu elimu ya vyuo vikuu nchini ambao wamekuwa wakilalamika kukosa nafasi za ajira
katika makampuni na mashirika mbalimbali.
Suala
la vijana hao kukosa ajira limekuwa
likiongezeka kadri siku zinavyosonga mbele na hivyo kuwa si geni tena miongoni mwetu na wala halina
kificho kwa sababu tumekuwa tukiwashuhudia kila siku wengi wao wakirandaranda
mitaani bila kazi maalumu.
Hali
hiyo hupelekea wengi wao kuingiwa na tamaa na kujikuta wakifanya vitendo viovu
ambavyo havikubaliki katika jamii ikiwamo uvunjaji wa sheria,utapeli na
kujihusisha na biashara haramu, ili wajipatie kipato cha kuendesha maisha yao.
Hata hivyo mfumo mbovu wa elimu bado ni kilio
cha watanzania wengi kutokana na kuzalisha wahitimu tegemezi wasio weza
kupambana katika soko la ajira za ndani na za kimataifa jambo ambalo hupelekea
ajira nyingi kuchukuliwa na wageni japo kuwa vyuo vyetu hapa nchini vimekuwa
vikizalisha wahitimu wengi kila mwaka.
Ili kutatua tatizo hilo Serikali kupitia Wizara
ya Kazi na Ajira, imekuwa ikibuni mipango mbalimbali ambapo hivi karibuni
ulizinduliwa mfumo maalum wa kielektroniki wa taarifa za ajira.
Licha ya
kuzinduliwa kwa mfumo huo lakini bado kuna umuhimu wa kujitathimini upya katika
suala la mfumo mzima wa elimu kwa kuwepo ongezeko la wastani wa 48% wanafunzi wanao
jiunga na elimu ya juu nchini lakini bado wengi humaliza wakiwa na elimu ya
nadhalia kuliko vitendo katika fani walizosomea na kuonekana hawana uwezo na
ubora katika soko la ajira ndani na nje ya nchi .
Katika kulitambua hilo, serikali kupitia
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, imeamua kuweka mkazo katika
suala hilo ili kuhakikisha kuwa utumishi wa umma unakuwa na watumishi wenye
weledi wa hali ya juu kupitia mchakato
wa ajira
Bi. Riziki Abraham ambaye ni msemaji wa
sekretarieti hiyo, anasema lengo la Serikali ni kuhakikisha inapata waombaji wenye sifa kitaaluma, uwezo na ujuzi
ili kuufanya utumishi wa umma unaendeshwa na watu wenye weledi na maadili mema
katika kuiwezesha serikali kutimiza malengo yake kwa ufanisi.
“Kwa kuwa nchi nyingi duniani na hususani
kwenye utumishi wa umma zimeweza kuendelea kwa kasi kubwa kutokana na kuwa na
Rasilimali Watu wenye kukidhi viwango na weledi wa hali ya juu, Rasilimali Watu
wenye sifa ni nguzo muhimu katika utendaji kazi ulio bora na wenye kufikia
malengo katika sehemu yeyote iwe za huduma au uzalishaji,”anasema.
Anasema upatikanaji wa Rasilimali watu bora
inategemea sana na uwepo wa wahitimu bora kutoka katika vyuo na taasisi za elimu ya juu zilizopo katika nchi husika.
“Baadhi ya wahitimu nchini humaliza ngazi mbalimbali za elimu na kutunukiwa
vyeti lakini hawana uelewa wa kutosha wa kile walichokisomea pia hukosa ufahamu
wa juu ya mambo yanayoendelea kwenye
mazingira husika, ”anafafanua.
Anasema wengi wa wahitimu hao hutarajia wawe na
uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa pindi wamalizapo masomo yao katika sekta
binafsi na zile za umma kutokana na weledi wa kuendana na soko la ajira katika
karne hii ya sayansi na teknolojia.
Bi. Abrahamu anasema kwa miaka minne sasa tangu
Sekretarieti ya Ajira ipewe jukumu hilo,
imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ubora wa wahitimu
wanaowasilisha maombi ya kazi serikalini kuanzia waombaji wenye elimu ya ngazi
ya Sekondari, Astashahada, Stashahada, Stashahada ya juu, Shahada, Shahada ya Uzamili
pamoja Shahada ya Uzamivu.
“Sekretarieti ya Ajira katika tathimini yetu
tumebaini mapungufu mbalimbali yatokanayo na ubora wa wahitimu wa ngazi mbalimbali
za elimu ya juu ambao huomba ajira kupitia chombo hiki na hata wale walioko kazini.
“Hata hivyo tofauti ya mapungufu yao
hutofautiana kutoka ngazi moja na nyingine, uwezo wa kitaaluma na ufahamu, kuamini
vyeti peke yake vinaweza kuwapa kazi pasipokuwa uelewa mpana wa kile walicho
ombea kazi, kutotilia maanani sifa au vigezo na masharti ya tangazo husika na kutokujiamini
pia.
kukosa
uzoefu kwa kazi inayohitaji uzoefu, uwezo mdogo wa mawasiliano ikiwemo
matumizi ya lugha sahihi, uwezo mdogo wa kutumia nyenzo za utendaji kazi
hususani vifaa vya kieletroniki, kutojiandaa vya kutosha, kukosa mbinu za
usaili na kutozingatia muda,” anasema.
Anasema changamoto nyingine ni kutokujitambua
kwa baaadhi ya wahitimu ambapo wengine husoma kwa kufuata mkumbo na hivyo kukosa
sifa halali za kitaaluma, kutokujua namna ya kuandika barua za maombi ya kazi, namna
ya kuandika wasifu wao (CV), kutokuwa na maandalizi sahihi pamoja na kughushi
baadhi ya sifa kwa lengo la kujipatia ajira.
“Wahitimu wanaoomba kazi wakitokea kazini
baadhi yao wameonyesha udhaifu wa kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na
changamoto hivyo kuona bora atafute kazi nyingine, kutokupitisha barua kwa
wajiri, kukosa uelewa mpana unaoendana na uzoefu wake kazini ili kuweza
kuonyesha tofauti yake na waajiri wapya, kukimbilia Serikalini ilikupata fursa
ya kusomeshwa lakini si kwa lengo la kwenda kuongeza tija kiutendaji,”anasema.
Bi. Abraham anasema hali hii inadhihirisha
kwamba wapo waombaji kazi ambao wanasoma ili kufaulu au kuhitimu na sio kuelewa
kwa ufasaha fani wanazosomea ili kuweza kuleta utaalamu wao katika nyanja
mbalimbali za maendeleo.
“Hali hii hupelekea kuchangia kushindwa kufikia
hatua ya kuitwa kwenye usaili kutokana na kukosa baadhi ya vigezo na wengine
kufikia hatua ya usaili na kushindwa kufaulu usaili husika kutokana na kutokujiandaa
ipasavyo,” anasema
Dkt. Benson Bana ni Muhazili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
katika kitengo cha rasilimali watu (human resouce), yeye anaonekana kwenda
tofauti na tathimini hiyo kwa kudai haijaangalia kwa undani changamoto
wanazosema wahitimu hao.
Anasema vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu
hutoa mafunzo kwa jumla kama maarifa yatakayo msaidia muhitimu, lakini mafunzo
ya kazi huyapata akiwa kazini.
“Wahitimu wetu ni bora tafauti na nchi zingine
ila ni juhudi za muajiri kuhakikisha anaandaa
mazingira mazuri na mafunzo ya kazi kwa vitendo kwa wale anaotaka kuwaajiri,
kiuwalisia uwezi kutarajia mwanafunzi anapomaliza miaka minne akawa weza kumudu mazingira kwa haraka.
“Kazi ya
vyuo ni kutoa maarifa na kuwaanda
wahitimu lakini elimu ya kazi anatakiwa kuipata akiwa kazini,”anasema Bana.
Anasema muhitimu hawezi kufanya kazi tofauti na
vigezo vinavyotakiwa na mwajili wake,
ukiona mpaka anaajiliwa anakuwa katimiza vigezo vyote na kwamba zipo taaluma
zinazo tegemeana kulingana muhitimu
alisomea kitu gani.
Anasema nchi yetu bado inatatizo la mbinu za
kutumia katika usaili kwa kuwa mbinu
nyingi zinazo tumiwa ni zakizamani na hazitoshi kuweza kujua uwezo wa mtu kwa
kuwa hata hao wanaosaili hawana uwezo na mbinu zao zimepitwa na wakati.
“Mimi kama mtaalamu wa rasilimali watu hapa nchini,bado tunahitaji kujipanga
kutafuta mbinu nzuri zaidi ya moja ambazo zitatusaidia kupata wahitimu na
watendaji kazi wanao hitajika,kwa kuwa mbinu zinazotumiwa zimepitwa na wakati katika
kufanya usaili na kutokana na mbinu hizo hatuwezi kupata watendaji wazuri kwa
kuwa hata hao wanao fanya usaili hawana uwezo unaotakiwa.
“Nimesha wahi kufanya kazi na sekretarieti ya
ajira hapa nchini, kwa hiyo najuwa uzahifu wao, usaili mwingi unafanyika kwa kutumia
njia moja tu ambayo ni maswali, na
utakuta hao wanao fanya usaili hawajapewa elimu ya kusaili inapelekea hata
maswali wanayo uliza kuwa tofauti na malengo ya kazi vilevile kingereza sio sehemu
ya kupata mtendaji mwadilifu kwa maana mtu
anaweza kujua kingereza bado akawa sio
mtendaji mzuri,” anasema Bana.
Anasema dunia ya leo
inahitaji mabadiliko, cheti ni kigezo cha kugundua kiwango cha elimu ya
muhusika na ni lazima mwajili ajue anatafuta mfanyakazi wa aina gani na awe tayari
kumuendeleza kwa kumpa mafunzo ya kazi ili mwajiriwa apate uzoefu na katika
kutekeleza hilo, ni lazima mwajili alifanye ipasavyo asikwepe wajibu wake.
Akichangia hoja hiyo, mwanafunzi
wa mwaka wa tatu, anayechukua shahada ya elimu katika chuo kikuu cha St john,
Nuru Masera, anasema baadhi ya vyuo na taasisi za elimu ya juu, wahadhili wake
wengi hawana viwango vinavyo hitajika na serikali.
“Baadhi ya vyuo
wanafundishwa na wahadhili ambao hawana viwango labda kwa kuwa wengi wamemaliza
degree, kinyume na agizo la serikali,pia vigezo vya ajira kwa waajiri wengi uwa vikubwa tofauti na hali alisi ambayo wahitimu wengi wanavyo, ” anasema
Masera.
Masera anasema licha ya
uzembe wa mwanafunzi mwenyewe katika kuakikisha anajisomea na kutambua
wajibuwake pia suala la semina ambazo zimekuwa zikiendeshwa katika vyuo nayo
inaonekana kualibu latiba ya mwanafunzi.
“Utakuta kipindi
kinaendelea uku mwanafunzi yupo kwenye semina labda anategemea amwombe mwenzie amuelekeze
baada ya kumaliza na kwa kuwa ratiba ya kipindi cha darasani na semina zimekuwa
sambamba anajikuta hana jinsi,”anafafanua.
Anasema kutokana na
baadhi ya taaluma hazipewi kipaumbele na serikali, wanafunzi hujikuta wanabadili
taaluma wanayosomea au kazi kutokana na
maslahi au mazingira ya kazi husika yalivyo.
“Wahitimu wengi
hujikuta wanafanya kazi kutokana na maslahi na mazingira duni kwa baadhi ya
ajira , ndio yanayopelekea wanafunzi kubadili taaluma wanayosomea na mwajili
hawezi kukuajili kama hautakuwa na vigezo anavyo vitaka kwa vile taaluma nyingi
hutegemeana,”anafafanua Masera.
No comments:
Post a Comment