Afrika inasherehekea miaka 50 ya umoja wa kisiasa na uchumi
unaonawiri, ambapo bara hilo kwa muda mrefu sasa linaangaliwa kama eneo la
neema kubwa, licha ya ukuaji huo wa kiuchumi kuwa na walakini.
Bara la Afrika linasherehekea hivi
sasa miaka 50 ya Umoja wa Afrika kwa ufanisi tangu wa kisiasa mpaka wa
kiuchumi. Bara hilo linajitokeza kama eneo lenye fursa kubwa ya kuwavutia
wawekezaji. Baada ya "Chui wa Asia" sasa Simba wa Afrika wananguruma.
Takwimu zinadhihirisha uchumi
utakuwa mwaka huu kwa 7% au zaidi katika robo ya mataifa yote ya eneo la kusini
mwa jangwa la Sahara. Wakati huo huo, mengi ya mataifa hayo yamo katika lile
kundi la mataifa ambayo uchumi wake unakuwa haraka kupita kiasi.
Waafrika wawili kati ya watano wana
simu ya mkononi au Smartphone. Nguvu za ununuzi zinazidi kukuwa barani Afrika
na masoko yanaongezeka, huku matajiri wakizidi kuongezeka barani humo. Huu ni
ufanisi wa kusisimua ambao watu wanapenda kuuzungumzia – naiwe wanasiasa,
wanauchumi na pia vyombo vya habari.
“Afrika inajikwamua“, anasema
mwandishi habari wa masuala ya kiuchumi Anver Versi. Mkenya huyo anaemiliki
jarida la kiuchumi la African Business Magazine linalochapishwa mjini London
anasema: "Kuna sababu nzuri za kuhoji kwamba Afrika itageuka kuwa soko
muhimu la ukuaji wa kiuchumi katika miaka 50 inayokuja .Kwa sababu Afrika ina
mali ghafi na nguvu kazi. Mtu anaweza kusema Afrika ni mahala pa kuvutia kabisa
kuwekeza hivi sasa - Wachina wameitambua hali hiyo tangu miaka 10 au 15
iliyopita. Na sasa wajasiriamali wa Kijerumani na wazungu kwa jumla wanabidi
wazindukane na kuitambua fursa hiyo."
Matumaini yana walakini
Katuni ya maadhimisho ya miaka 50 ya
Umoja wa Afrika.
Kwa mujbu wa makadirio ya Benki Kuu
ya Dunia, uchumi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara utakuwa kwa kadiri
ya 5% katika kipindi cha mwaka 2013 na 2015. Uchumi wa dunia katika kipindi
hicho hicho utakuwa kwa kadiri ya 3% tu.
“Viwango hivyo ni vya juu vya ukuaji
wa kiuchumi, lakini hiyo bado si sababu ya kushangiria,“ anasema Robert Kappel.
Mtaalam huyo wa Kijerumani anayeshughulikia masuala ya utafiti wa masuala ya
Afrika katika taasisi ya GIGA mjini Hamburg, amechunguza makadirio ya ukuaji wa
kiuchumi katika mataifa 42 ya kusini mwa jangwa la Sahara. Mengi ya mataifa
hayo hayatofua dafu kwa mlinganisho wa kimataifa.
Robert Kappel anasema: "Ukuaji
unatokana zaidi na ile hali kwamba mahitaji ya mali ghafi na bidhaa za
mashambani yameongezeka sana katika kipindi cha miaka iliyopita na kwa namna
hiyo bei nazo zimepanda. Kwa hivyo, inamaanisha biashara ya nje inachangia sana
katika ukuaji wa kiuchumi barani Afrika na huo ni udhaifu mkubwa."
Taasisi kuu za fedha duniani,
Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki Kuu ya Dunia, zote zinaonya juu ya bara
la Afrika inategemea sana biashara na nchi za nje. Naye Katibu Mkuu wa zamani
wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, aliyataka mataifa ya viwanda katika Kongamano
la Kiuchumi la Kimataifa hivi karibuni mjini Cape Town nchini Afrika ya Kusini
yawekwe sheria kali katika biashara ya mali ghafi pamoja na Afrika. “Rushwa na
kukwepa kulipa kodi za mapato,“ anasema Kofi Annan, “ndio chanzo cha kudhoofika
neema barani Afrika.“
Nini cha kufanya kuimarisha uchumi?
Mchoro wa maadhimisho ya miaka 50 ya
Umoja wa Afrika.
Shughuli za viwanda zinazorota
barani Afrika na kilimo hakitoshi hata kukidhi mahitaji ya wakaazi wa bara
hilo. Hata katika soko la ajira hakuna ishara ya kuongezeka nafasi za kazi.
Hata katika nchi inayonyanyukia kiuchumi ya Afrika ya Kusini, zaidi ya 25% ya
wakaazi wake hawana kazi na wanaoathirika zaidi ni vijana wanaoishi mashambani.
Kwa hivyo, nini cha kufanya ili
ukuaji wa kiuchumi barani Afrika utuwame katika msingi imara? Mwandishi habari
wa masuala ya kiuchumi, Anver Versi, anahisi panahitajika vitega uchumi zaidi
katika miundo mbinu. Naye Robert Kappel wa Taasisi ya Uchunguzi wa Masuala ya
Afrika anahisi mageuzi ya kiuchumi pia yanahitajika pamoja na sheria bora za
uwekezaji ili kuwavutia wateja tangu wa ndani mpaka wa kimataifa.
No comments:
Post a Comment