MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kwa mara ya kwanza ameibuka
na kupingana na harakati za Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Zitto
amesema hana uhakika wala hauamini Ukawa kama utakuwa umoja endelevu
hadi kufikia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwa sababu si mara ya kwanza
vyama vya upinzani kuungana na kugawanyika.
Mbali
ya kutokuwa na imani na umoja huo, pia ameitaka Serikali kusitisha
mchakato wa Katiba Mpya hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika.
Alisema ni vema mchakato huo ukasitishwa kwa sasa, kwani inaonekana wajumbe wa Bunge hilo wanafuja fedha za umma.
Zitto
alitoa kauli hiyo juzi, wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power
Breakfast kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds cha jijini Dar es
Salaam.
Alisema Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi na si Katiba pekee.
Alisema
siku zote Watanzania wamekuwa wakipenda kuwa na upinzani imara ambao
watu wanaweka tofauti zao pembeni na kuungana dhidi ya chama ambacho
kinaongoza, lakini haoni kama Ukawa utaendelea hadi kufikia kipindi cha
Uchaguzi Mkuu.
Alisema
hatua ya kusimama kwenye ajenda moja ya Katiba haitausaidia umoja huo,
kwani kipindi cha uchaguzi mkuu kinakuwa na ajenda nyingi.
Alisema wananchi watapenda kusikia masuala ya kushughulikia rushwa, matumizi ya rasilimali, maji, umeme, afya na barabara.
“Mambo haya ndiyo yatakayowafanya wananchi waamue namna gani watakabidhi dhamana ya uongozi, si suala la Katiba pekee,” alisema Zitto.
Alisema tusijitoe ufahamu kwa kudhani kwamba hii ndio mara ya kwanza kwa upinzani kuungana.
“Kulikuwa
na Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (KAMAKA) pia katika chaguzi za mwaka
1995, mwaka 2000 wapinzani waliungana vilevile, lakini kila inapokaribia
uchaguzi wamekuwa hawaelewani kwa kuwa kila mtu anataka chama chake
kipeperushe bendera.
“Lakini
kama Ukawa wataweza kuweka ajenda yao mpaka mwisho itakuwa jambo jema
kwa wananchi wenyewe. Kwa sababu nchini kwetu tatizo kubwa ni usimamizi
na uwajibikaji, kama ajenda itachukua nafasi naamini hali haitakuwa
mbaya, lakini bado siamini na sina uhakika kama umoja huu ni endelevu
kwa namna ambavyo tunaona, ni umoja ambao unatokana na matakwa ya sasa
ya Katiba, wameungana kwa sababu ya serikali tatu, lakini aina gani ya
serikali bado hili linaweza kuwagawa,” alisema.
… mchakato wa Katiba Mpya usitishwe
Akitolea
ufafanuzi hoja yake ya kusitisha mchakato wa Katiba Mpya, Zitto alisema
ni vyema serikali ikausitisha ili kunusuru fedha za umma zisiteketee.
Alisema
fedha hizo zinastahili kutumika kununua madawa, kuendeleza miradi ya
maji na kusomesha Watanzania, hivyo hakuna sababu fedha hizo kutumika
kwa ajili ya kupiga porojo na kutukanana ndani ya Bunge.
“Nashauri
tuahirishe mchakato huu mpaka baada ya uchaguzi mkuu mwaka kesho, ndipo
hapo tuwe na mamlaka ya kujadili mchakato huu na kumaliza.
“Pia
uchaguzi unaweza kuchekecha na ukaondoa baadhi ya watu ambao ni vikwazo
katika mchakato kwa sababu uchaguzi hauna muamala, mtu ambaye alikuwa
mbunge anaweza kuondolewa,” alisema.
Aidha,
alisema kabla ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu, Katiba ya sasa inatakiwa
kurekebishwa baadhi ya maeneo ambayo ni vikwazo, kama vile Tume huru ya
uchaguzi, kipengele cha wagombea binafsi kiwekwe na maeneo ambayo
Zanzibar wamekuwa wakiyahitaji katika Katiba mpya, kwa mfano suala la
mafuta na gesi yawekwe.
Alisema hakuna sababu ya kugawa nchi na kutumia rasilimali zilizopo kwa kufanya kazi ambayo haina matunda.
…amtetea January
Katika
hatua nyingine, Zitto, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
alisema amesikitishwa na mashambulizi yanayoelekezwa kwa Mbunge wa
Bumbuli (CCM), Januari Makamba, baada ya kutangaza nia ya kuwani urais
mwaka 2015.
Alisema
kila kijana anapojitokeza kwa ajili ya kutaka kushiriki katika mamlaka
za nchi, hasa katika nafasi kama hiyo ya urais, kumekuwa na mashambulizi
makubwa dhidi yake.
“Ni
hatua ambayo sio nzuri kwa sababu kwa mujibu wa takwimu, idadi ya watu
asilimia 72 wapo chini ya miaka 30, asilimia 65 ya wapiga kura ni vijana
wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 40, hivyo vijana wana haki ya
kushiriki katika uongozi wa nchi, tufahamu changamoto za maendeleo ya
nchi yetu zinahitaji uongozi mpya wa kizazi kipya.
“Ni
dhahiri neno ujana si sifa, lakini neno uzee pia si sifa, hivyo
tunatakiwa kuwapima vijana kwa sifa zilizopo, kama vile za kikatiba na
zile za ziada, badala ya kusema vijana hawajakomaa… nilisikitika sana na
mashambulizi ambayo yalielekezwa dhidi ya Makamba, natoa wito kwamba
tuache, kwani wenye uamuzi wa mwisho ni wananchi.
“Mtu
akigombea na kama akitoa sera zake vizuri wananchi wakamwelewa,
akichaguliwa ni wananchi wameamua, hakuna mtu mwenye mamlaka kuwa fulani
ni kijana, nadhani lazima tubadilishe uongozi na watu wajue nchi hii ni
ya vijana, hatusemi wazee hawawezi ila wao wabaki kuwa washauri kama
wao walivyokuwa vijana katika kipindi cha Nyerere nao walikuwa na miaka
40. Hivyo kuna haja ya kuweza kufikia hapo, changamoto za nchi ni kubwa,
kuna haja ya aina mpya ya uongozi na mimi naamini aina hiyo itatoka kwa
viongozi vijana,” alisema.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Zitto, ambaye yuko ndani ya Chadema kwa sababu za kisheria, kuibuka na kuuzungumzia Ukawa.
Mwanasiasa
huyo kijana amekuwa kimya kwa muda mrefu, hata kwenye harakati za Ukawa
amekuwa aghalabu kuonekana, hali ambayo imekuwa ikiibua maswali yuko
upande gani katika mchakato huu wa Katiba Mpya.
Kauli
hii ya Zitto inaweza kuibua fikra mpya kwa baadhi ya watu ambao
wamekuwa na imani kubwa na umoja huo unaoviunganisha baadhi ya vyama vya
siasa nchini.