![]() |
Rais Putin akimpokea Rais Al-Sisi, Sochi |
Rais wa Urusi, Vladmir Putin amekutana na mwenzake wa Misri, Abdel
Fattah al-Sisi, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana kuhusu
masuala ya ushirikiano mkubwa wa kijeshi, teknolojia na biashara huria.
Putin amesema mwezi Machi mwaka huu nchi hizo mbili zilisaini itifaki zinazolingana na kwamba wanapeleka silaha nchini Misri na wako tayari kutanua ushirikiano huo.
Aidha, Al-Sisi amemshukuru Rais Putin kwa kuwa kiongozi wa kwanza nje ya mataifa ya Kiarabu, kumualika tangu alipoapishwa kuliongoza taifa lake. Alisema watu wote wa Misri wanaifatilia ziara yake na wanategemea kuwepo kwa ushirikiano wa hali ya juu kati ya mataifa hayo mawili.
Urusi imechukua jukumu la kupeleka silaha Misri, baada ya Marekani kusitisha kupeleka silaha kutokana na ukandamizaji uliofanywa na Al-Sisi baada ya kuiondoa madarakani serikali ya zamani ya Kiislamu, mwaka uliopita.
Baada ya mkutano wa viongozi hao wawili, gazeti la kila siku la biashara la Urusi la Vedemosti limeripoti kuwa Urusi na Misri zimesaini mpango unaokaribia Euro bilioni 2.2 wa makombora na ndege za kivita, utakaofadhiliwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Misri inapendelea zaidi mifumo ya ulinzi wa anga
Mkuu wa kituo cha utafiti wa biashara ya silaha duniani mjini Moscow, Igor Korotchenko, amesema Misri inapendelea zaidi mifumo ya ulinzi wa anga. Amesema anadhani kusainiwa kwa mikataba halisi ni suala la muda tu na kwamba makubaliano katika ngazi ya kisiasa tayari yameshafikiwa.
Ama kwa upande mwingine, Rais Putin ameikaribisha Misri kuanzisha ukanda wa biashara huru kati ya Misri na umoja wa ushuru na forodha wa Urusi, Belarus na Kazakhstan. Urusi imesema itaongeza kiwango cha kupeleka ngano nchini Misri na kuingiza bidhaa nyingine za kilimo kutoka Misri.
Urusi inaangalia vyanzo vipya vya usambazaji wa bidhaa, baada ya wiki iliyopita kupiga marufuku chakula kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Australia, Canada na Norway, ikiwa ni katika kujibu hatua ya vikwazo vilivyowekwa dhidi yake kutokana na mzozo wa Ukraine.
Akizungumza baada ya kukutana na Rais Al-Sisi, Putin amesema tayari Misri imeongeza usambazaji wa bidhaa za kilimo kwenye soko la Urusi kwa asilimia 30 na iko tayari kuongeza asilimia nyingine 30 katika siku zijazo.
Waziri wa Kilimo wa Urusi, Nikolai Fyodorov, amewaambia waandishi wa habari mjini Sochi kuwa kuongezeka kwa chakula kama vile viazi, vitunguu, vitunguu saumu na machungwa kutoka Misri, kutasaidia kufidia nusu ya upungufu wa bidhaa hizo uliosababishwa na hatua ya kupiga marufuku.
No comments:
Post a Comment