Tuesday, 12 August 2014

Cadema imewataka wazee washirikiane ili kutetea maslahi yao na Taifa

MWENYEKITI  wa  Chama  cha  Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Temeke, Bernard Mwakyembe  amewataka wazee nchini kuongeza ushirikiano ili kutetea maslahi yao na taifa kwa ujumla kutokana na busara walizonazo.  
Rai hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana,  wakati wa semina ya kutambua sifa za kiongozi bora iliyowakutanisha zaidi ya wazee 100.
Mwakyembe alisema, hakuna jambo lolote linaloweza kufanikiwa bila ya kushirikisha kauli za wazee, hasa waliokuwa na busara katika utatuzi wa mambo mbalimbali ikiwemo migogoro katika vyama.
“ Kauli ya wazee ni dawa, lakini kutokana na kuwa nyuma kwenye suala la kujitolea wanaonekana hawafai au wamepitwa na wakati, haya yote huenda yakatokana na wengi wao kutotambua sifa zao katika jamii inayowazunguka”alisema.
Mwakyembe aliwahakikishia wazee hao kuwa, Chadema itasimamia haki zao juu ya kuzitambua sifa zao zitakazowasaidia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuleta mabadiliko yatakayowainua kiuchumi.
Hata hivyo, aliwafafanulia baadhi ya sifa anazostahiki kuwa nazo kiongozi kuwa, awaze mafanikio makubwa, awe na nia kwa jambo analotaka kuongoza, ajitambue mwenyewe, asimamie maamuzi sahihi asiwe kigeugeu pia adhibiti msongo wa mawazo.
“Siku zote uongozi ni dhima kuna wale wanaozaliwa  na bahati hiyo huku wengine wakizisomea, lakini yote sawa hivyo kiongozi bora
anatakiwa akubali kukosolewa, awe msikilizaji na afuate haki, pia anatakiwa atie moyo watu pamoja na kufurahia mafanikio”alisema.
Alisema, kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wasaliti kutoka na kutozingatia sifa za uongozi ikiwemo kukubali lawama, kutoungana na watu wa chini yake, kushindwa kutatua matatizo, kutojifunza kutokana na makosa pamoja na kukosa uaminifu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wazee wilayani humo, Waziri Mkunguna aliwataka wazee wenzake kuhakikisha wanajitolea katika mambo mbalimbali ya kukiendeleza chama hasa kwa kuzingatia kanuni na sifa walizoambiwa.
MWISHOO.

No comments:

Post a Comment