Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limewakamata watu watano wakiwa na
magunia saba ya madawa ya kulevya aina ya bhangi wakiwemo mke na mume.
Awali askari wa Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya Mkoani hapa wakiwa
doria walipata taarifa toka kwa raia wema iliyoeleza kuwepo kwa watu
wanaosafirisha madawa hayo.Mara baada ya kupata taarifa hiyo askari hao waliweka mtego maeneo ya Sanawari ambapo muda wa saa 3:30
usiku walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Hussein Rashid
(35) mkazi wa Sakina, dereva pamoja na mwenzake Sebastian Wilbert (37)
Fundi magari, mkazi wa Ilboru wakiwa wanasafirisha magunia matano ya
madawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogramu 171 kuelekea
nchi jirani ya Kenya kwa kutumia gari aina ya Toyota Corolla lenye namba
za usajili T. 589 AZS.
Gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T.589 AZS
likiwa limebeba magunia ya madawa ya kulevya aina ya bhangi mara baada
ya kukamatwa eneo la Sanawari jijini Arusha na askari wa kitengo cha
kuzuia Madawa ya Kulevya mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi
la Polisi Arusha) Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema
kwamba, mara baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa walikiri kosa hilo na
kumtaja mwanamke aitwaye Flora John (38) Mkazi wa Ekenywa- Ngaramtoni
kuwa ndio aliyewauzia.
Kamanda Sabas aliendelea kwa kusema kwamba, askari hao walianza
kumfutilia mwanamke huyo ambapo jana Jumanne tarehe 05.08.2014
walikwenda nyumbani kwake na kumkuta mtuhumiwa ambaye ni muuzaji akiwa
na mume wake aitwaye John Meleji (45) Mkazi wa Ekenywa na mara baada ya
kufanya upekuzi walikuta gunia moja la madawa ya kulevya aina bhangi
ndani ya nyumba hiyo.
Mbali na kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni mke na mume pia askari
hao walimkamata jirani yao aitwaye Loseriani Metelami (21) Mkulima mkazi
wa Ekenywa baada ya yeye pia kukutwa na gunia moja la madawa ya kulevya
aina ya bhangi hivyo kufanya jumla ya magunia yaliyokamatwa kuwa saba.
Watuhumiwa hao watano wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni mara baada ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment