Wednesday, 3 September 2014

TTCL wabainisha mkongo wa mawasiliano umepunguza gharama za mawasiliano kutoka 36000/gb mwaka jana hadi 9000/gb mwaka huu



WIZARA  ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda mkongo wa Taifa kwani kumekuwa na desturi ya baadhi yao kuuchimba wakidhani wanaweza kupata chuma chakavu.
Mbali na hilo imesema kwamba mkongo huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za mawasiliano ambapo awali gharama za intaneti zilikuwa 36000/GB hadi 9000GB mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Afsa uhusiano wa Wizara hiyo Prisca Ulomi alisema kwamba ni jukumu la kila mwananchi kuutunza mkongo huo ambao umegharimu fedha nyingi za Serikali kwani ni wetu sote. 
Alisema Mkongo huo ambao kwa sasa wanaingia katika awamu ya tatu ukikamilika utasaidia watoa huduma kufikisha huduma za mawasiliano  haraka na uhakikika na kwa gharama nafuu.
“Hata hivyo itaharakisha maendeleo ya Taifa kwa kuwa wananchi watapata fursa ya kutumia TEHAMA katika juhudi za kupambana na umaskini na kujiletea maendeleo kwa kasi zaidi ambapo hadi sasa inaonyesha kwamba asilimia 10 ya matumizi ya Tehama nchini yanachangia kwenye pato la Taifa kwa kiasi cha asilimia 1.38.
“Pia Mkongo wa taifa unatoa muunganisho wa mawasiliano kwa nchi zote za jirani hasa zile ambazo hazipakani na bahari ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi, pia mkongo umeiunganisha Tanzania na Mikongo ya baharini ya SEACOM na EASSY”alisema.


No comments:

Post a Comment